RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA


Rais wa Jamhuri ya Cabo Verde, Mhe. José Maria Pereira Neves, amezihimiza nchi za Afrika kuimarisha demokrasia na utawala bora ili kuepuka kurudia makosa ya kihistoria yaliyoletwa na ukoloni, ambayo hadi sasa yameziacha baadhi ya nchi zikiendelea kudai fidia.


Mhe. Neves alitoa kauli hiyo alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mwaka Mpya wa Mahakama ya Umoja wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, hafla iliyofanyika jijini Arusha. Alionya kuwa migogoro inayoendelea kushuhudiwa barani Afrika inaathiri maendeleo ya kijamii, huku sababu kuu ikiwa ni ukosefu wa haki za binadamu na uongozi bora.


“Naipongeza Mahakama ya Umoja wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa kuchagua kaulimbiu inayosisitiza ulipaji wa fidia kama njia ya kuendeleza haki kwa watu wa Afrika. Hata hivyo, fidia ni zaidi ya malipo ya kifedha—ni mchakato wa uponyaji wa majeraha ya kihistoria. Hatutakiwi kuishia kulaani na kukemea tu, bali tunapaswa kuchukua hatua za kweli. Vinginevyo, vizazi vijavyo vitadai fidia si kwa wakoloni, bali kwa migogoro tunayoendelea kuianzisha sisi wenyewe,” alisema Rais Neves.


Awali, Rais wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Imani D. Aboud, alibainisha kuwa kaulimbiu ya mwaka huu imezingatia dhamira ya mahakama hiyo ya kuhakikisha watu waliopitia au wanaoendelea kupitia ukandamizaji wa haki zao wanapata fidia wanayostahili.


Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo majaji na wawakilishi wa taasisi za utetezi wa haki za binadamu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliwakilishwa na Naibu Waziri, Mhe. Dennis L. Londo (Mb.), ambaye alimwakilisha Waziri Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Said Shaib Musa, pia alihudhuria.


Ufunguzi wa Mwaka Mpya wa Mahakama ya Umoja wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu umefanyika katika Makao Makuu ya Mahakama hiyo jijini Arusha, tarehe 3 Februari 2025.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI