Jumamosi tarehe 26 Februari, 2022. Urusi inatekeleza kile alichokiita Rais wa nchi hiyi Vladimir Putin 'Operesheni Maalumu' nchini Ukraine aliyoitangaza siku ya Alhamisi tarehe 24 Februari, 2022. Wakati huu ambapo Urusi ikielekea Mji Mkuu wa Ukraine Kyiv Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameomba nchi za Muungano wa Umoja wa Kujihami Kaskazini mwa Bahari ya Atlantiki (NATO) uweze kumsaidia lakini hakuna nchi hata moja iliyojibu ombi hilo. Makala hii inaangazia sababu za Urusi kuingia nchini Ukraine na uhalisia wa NATO kuweza kuisaidia Ukraine isikutane na athari zaidi ikiwemo kutwaliwa kwa Mji Mkuu Kyiv na athari za vikwazo ilivyowekewa Urusi kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya. Chanzo cha Vita Chanzo cha Vita/ Mgogoro na uvamizi huu wa sasa wa Urusi kinatokana na tishio la kiusalama linaloletwa na NATO dhidi ya Urusi. Tishio hili lilianza kushika hatamu mara baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Viktor Yanukovych Februari, 2014. Rais Yanukovych aliondolewa madarakani...