VITA YA URUSI DHIDI YA UKRAINE NA UKWELI KUHUSU NATO
Jumamosi tarehe 26 Februari, 2022.
Urusi inatekeleza kile alichokiita Rais wa nchi hiyi Vladimir Putin 'Operesheni Maalumu' nchini Ukraine aliyoitangaza siku ya Alhamisi tarehe 24 Februari, 2022.
Wakati huu ambapo Urusi ikielekea Mji Mkuu wa Ukraine Kyiv Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameomba nchi za Muungano wa Umoja wa Kujihami Kaskazini mwa Bahari ya Atlantiki (NATO) uweze kumsaidia lakini hakuna nchi hata moja iliyojibu ombi hilo.
Makala hii inaangazia sababu za Urusi kuingia nchini Ukraine na uhalisia wa NATO kuweza kuisaidia Ukraine isikutane na athari zaidi ikiwemo kutwaliwa kwa Mji Mkuu Kyiv na athari za vikwazo ilivyowekewa Urusi kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya.
Chanzo cha Vita
Chanzo cha Vita/ Mgogoro na uvamizi huu wa sasa wa Urusi kinatokana na tishio la kiusalama linaloletwa na NATO dhidi ya Urusi.
Tishio hili lilianza kushika hatamu mara baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Viktor Yanukovych Februari, 2014.
Rais Yanukovych aliondolewa madarakani kwa mapinduzi yaliyoungwa mkono na kusaidiwa na Nchi za Magharibi baada ya kukataa kusaini Mkataba wa Ushirikiano na Soko Huria na Umoja wa Ulaya na badala yake kujielekeza zaidi Urusi kwa kupatiwa msaada wa fedha na nchi hiyo. Rejea Congressional Research Service Report ya Oktoba 5, 2021 kubaini hili.
Hali hiyo ilisababisha kutokea kwa maandamano makubwa na hatimaye Mapinduzi yaliyojulikana kama Mapinduzi ya Heshima (Revolution of Dignity) mwezi Novemba, 2013 ambayo yalipelekea Rais Yanukovych kukimbilia Moscow mwezi Februari, 2014. Hapo ndipo Urusi ilipoanza Vita na Ukraine kwa kulivamia na kulitwaa kwa nguvu eneo la Crimea ambalo linaelezwa kuwa na wakazi wengi wenye asili ya Urusi. Rejea tena Congressional Research Service Report ya Oktoba 5, 2021.
Kwa kulitwaa eneo la Crimea Urusi inaamini kumepunguza ushawishi na athari za NATO na hasa Marekani katika eneo la Bahari Nyeusi na Bahari ya Caspian.
Lakini licha ya kufanya hivyo kwa miaka kadhaa sasa Urusi imekuwa ikiendelea kuhofu namna NATO inavyojipanua kueleka eneo la Mashariki mwa Ulaya kwa kupenyeza ushawishi kwa nchi za Georgia, Ukraine na Belarus kimkakati.
Kujipanua huku kwa NATO kunaelezwa na Kremlin kuwa na athari kubwa za kiusalama kwa Urusi katika eneo la mpaka wake wa Mashariki mwa Ukraine na hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa wigo wa ushawishi eneo lote la Ulaya Mashariki na Kusini mwa Caucasus.
Mkakati wa Urusi katika vita hii umejikita katika namna tatu:
Mosi, kupunguza ukubwa wa mpaka wa Ukraine. Kwa kawaida ukubwa wa mpaka wa nchi hutoa tafsiri ya namna nchi hiyo inakavyokuwa ngumu kuivamia kama alivyobainisha Sheehan (1996) katika 'The Balance of Power: History and Theory' kuwa mpaka wa nchi ni element muhimu sana katika Vita na hasa katika kutafsiri umbali wa kuifikia Ikulu ya Nchi.
Hii ndiyo sababu Ikulu nyingi za nchi huwa katikati ya nchi ili kuondoa athari za kufikiwa kwa urahisi na maadui.
Mkakati wa pili ni kuyakamata na kuyakalia maneo ya Luhansk na Donetsk kwa kutumia Serikali zinazoendeshwa nyuma ya pazia na Urusi.
Luhansk na Donetsk ni maeneo ambayo kwa miaka takribani minane sasa Urusi imekuwa ikijenga ushawishi yajitenge kutoka Ukraine. Kujitenga kwa maeneo hayo kuna athari kubwa kwa uchumi wa Ukraine.
Urusi imetekeleza mkakati huo kwa kuyatambua maeneo hayo kama nchi huru kupitia kwa makundi yaliyojitenga ya Donetsk People’s Republic kwa kifupi DPR na Luhansk People’s Republic au LPR tarehe 22 Februari, 2022.
Maeneo haya mawili kwa pamoja yanaunda eneo la Donbas ambalo ni muhimu sana kwa uchumi wa Ukraine kwa kuwa na viwanda vingi na machimbo ya makaa ya mawe.
Hivyo 'kuyakalia' maeneo hayo ni kuuvunja nguvu uchumi wa Ukraine.
Haya yalibainishwa pia na Wasielewski na Jones (2022:2) katika andiko lao 'Russia’s Possible Invasion of Ukraine' kwamba kitendo cha Urusi kuyamega na kuyatwaa maeneo ya Ukraine kutaivunja nguvu za kiuchumi nchi hiyo na kuiongezea Urusi nguvu kazi, uwezo wa viwanda na maliasili ambazo zitaifanya Urusi kuwa nchi tishio kwa dunia.
Kwa upande mwingine kuyakalia maeneo hayo kunapunguza zaidi mpaka wa Urusi na Ukraine kuelekea Ikulu ya Ukraine mjini Kyiv kutokea upande wa Mashariki na hivyo kuiweka Ukraine katika hatari zaidi.
Mkakati wa Tatu ni kuilazimisha Ukraine isijiunge NATO.
Urusi inatekeleza hili kwa kukamata maeneo ya Magharibi la Mto Dnepr, Odessa mpaka Transdniestria ili kuiathiri kiulinzi na kiuchumi Ukraine kwa kuinyima uwezekano wa kutumia Bahari Nyeusi.
Sambamba na hilo lengo ni kukamata pia maeneo ya Mariupol, Kherson naOdessa. Urusi inaamini kuwa maeneo hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kuwapatia maji wananchi wa Crimea huku Ukraine ikizuiwa isipate mwanya wa kutumia bahari.
Hayo yote yanalenga kuifanya Ukraine ikose njia nyingine zaidi badala yake ilazimike kukaa kwenye meza ya makubaliano kule Minsk, Belarus na 'kujitia kitanzi.'
Ni ipi nafasi ya NATO?
Kikanuni NATO inakosa muktadha wa kisheria kuingia Ukraine na kuilinda nchi hiyo.
Hili liliwekwa bayana na Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg mara baada ya kufanya mkutano na viongozi wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja huo kwa njia ya video tarehe 25 Februari, 2022 na badala yake viongozi hao wamekubaliana kupeleka vikosi na silaha kwenye nchi za Poland na Latvia ambazo ni wanachama wa NATO.
Kwa nini wapeleke vikosi na silaha Poland na Latvia?
Kimsingi NATO ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa (tazama collective defense) wa mwaka 1945 haiwezi kwenda kuingia kwenye nchi ambayo si mwanachama wake kulinda usalama pasina kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Endapo Ukraine ingekuwa imetia saini Mkataba wa kuanzishwa kwa NATO wa tarehe 4 Aprili, 1949 leo hii vita ya Urusi na Ukraine ingekuwa kubwa sana na huenda ingechukuwa muda mrefu zaidi kwa sababu ingekuwa mwanachama na hivyo Ibara za 5 na 6 za Mkataba huo zingeihusu Ukraine.
Kutokana na hilo NATO inawiwa vigumu kupeleka vikosi na silaha kwa kuepuka gharama ambazo itakuwa ngumu kuzithibitisha.
Ugumu mwingine wa NATO kuingia Ukraine unatokana ukweli kwamba kwa kuwa Ukraine si mwanachama wa NATO maamuzi ya nini kifanywe yanatoka Umoja wa Mataifa kupitia Baraza la Usalama la Umoja huo (UNSC) kwa kupiga kura kupitisha Azimio la kuilinda Ukraine.
Kikanuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hufanya kazi zake kwa kuzingatia Ibara ya 39, 40, 41, 42 na 43 za Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Kwa mfano mara baada ya kupitishwa Azimio namba 1973 mwaka 2011 ambalo lilitoa wajibu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kulinda raia nchini Libya (Responsibility to Protect -R2P) NATO iliwashiwa taa za kijani kupitia ibara ya 43 ya Mkataba huo wa Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wa hili la Azimio la Baraza la Usalama ni kikwazo cha kusuluhisha mzozo huu kwa sababu mbili, mosi nchi iliyo katika Vita ni muhusika mkuu wa kuamua maamuzi ya Baraza la Usalama. Pili, upigaji wa kura kupitisha Azimio hautoi nafasi kwa Ukraine kusaidiwa.
Ukweli upo hivi; Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) lina wanachama 15 ambao wamegawanyika katika makundi mawili:-
(1) Wanachama watano wa Kudumu
(2) Wanachama 10 wa Kawaida ambao hupatikana kwa mzunguko wa kinchi na mgawanyiko wa kikanda.
Mfano wa wanachama wasio wa kudumu ni nchi ya Kenya ambayo inaiwakilisha Afrika kupitia Balozi Kimani.
Kikwazo kwa Ukraine ni kura ya Turufu (VETO)
Veto ni hadhi ya kura yenye maamuzi ya mazito ama ya mwisho katika maazimio mbalimbali yanayopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).
Hadhi hii ya Kura ya Turufu (Veto) imepewa kwa upendeleo kwa mataifa matano ambayo yanaitwa wanachama wa kudumu wa Umoja wa Mataifa.
Mataifa haya yamepewa hadhi hiyo kutokana na mchango wao mkubwa uliopelekea kuundwa kwa Umoja wa Mataifa.
Mataifa haya ni pamoja na Uingereza, Ufaransa, Marekani, China na Urusi iliyorithi hadhi hii toka kwa iliyokuwa USSR.
Upigaji wa Kura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Upigaji wa kura za kuidhinisha Azimio lolote la Umoja wa Mataifa katika usuluhishi wa migogoro huhitaji angalau kura 9 kutoka miongoni mwa wajumbe 15 wa Baraza la Usalama.
Katika kura hizo 9 kusitokee nchi mwanachama wa kudumu ikapiga kura ya HAPANA, Azimio hilo haliwezi kupata utekelezaji wenye mantiki hata kama litapata kura zaidi ya 11 za kuliwezesha kupelekwa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Nani anadhani Urusi itapiga kura kuidhinisha NATO waingie Ukraine?
Kwa msingi huu hawa wanachama wa kawaida 10 ni kama hawana umuhimu wowote katika maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ni kama picha tu zimekaa pale, huo ndiyo ukweli.
Kimsingi mataifa hayo matano hufanya maamuzi ya NDIYO ama HAPANA kulingana na jinsi gani yana maslahi katika Azimio lililopo mbele yao.
Ndiyo maana Rais Joe Biden wa Marekani aliliona hilo mapema na kusema hatopeleka vikosi Ukraine , watu walimshangaa walimuona kama mtu muoga, la hasha! Alijua ugumu ulipo. Ni katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ni wazi kuwa ikiwa nchi inayojadiliwa ina maslahi ya moja kwa moja na jambo husika kama ilivyo kwa Urusi hupiga kura ya HAPANA kuzuia Azimio kupita.
Je kwa namna Baraza la Usalama lilivyo, Ukraine itapona?
Lakini udhaifu huu wa Baraza la Usalama unaleta maswali ya kisheria hasa kuzingatia kanuni za asili za haki (Principles of Natural Justice) hasa 'Nemo judex in causa sua' ambayo inaweka wazi kuwa upande hauwezi kushiriki katika kufanya maamuzi juu ya jambo ambalo una maslahi nalo.
Urusi imeingia vitani dhidi ya Ukraine kwa sababu ina maslahi na nchi hiyo kwa kuzingatia hofu ya nchi hiyo kujiunga NATO na hivyo Urusi kuwa kwenye hatari ya kupoteza biashara yake ya gesi nchini Ukraine na nchi nyingine za Ulaya ikiwemo Ujerumani. Je Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa si kikwazo kwa amani?
Vikwazo vilivyowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya vitasaidia?
Jibu ni kuwa vitasaidia lakini baada ya muda mrefu sana. Lakini yafaa tujiulize mpaka muda huo ambao vikwazo vitaanza kuonesha athari Ukraine itakuwa wapi?
Tafiti nyingi zinaonesha wazi kuwa vikwazo vimekuwa havina athari tarajiwa ukilinganisha na nia au malengo ya nchi.
Hii ndiyo sababu Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameweka bayana kuwa vikwazo pekee havitoshi bali nchi washirika zinapaswa kufanya zaidi ya hapo.
Kwa mfano Smeets (2018) katika andiko lake 'Can economic sanctions be effective?' lililotoka katika ripoti ya tarehe 15 Machi, 2018 ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) anabainisha kwa kusema kuwa takwimu za vikwazo vya kiuchumi kuwa na athari ni dhaifu mno.
Smeets anakubaliana na Hufbauer na wenzake (1990) kwa kuweka baya kuwa vikwazo vina kiwango kidogo cha kuwezesha kufikiwa kwa lengo la kuiathiri nchi husika akitoa mfano wa Urusi yenyewe ilipowekewa vikwazo 2014 na Iran ambayo iliwekewa vikwazo kadhaa tangu 1979.
Rejea zaidi:
Sakwa, R (2016) Frontline Ukraine: Crisis in the Borderlands I.B. Tauris
Kofman .M et al.,(2017) Lessons from Russia’s Operations in Crimea and Eastern Ukraine (RAND Corporation
Charap, S na Colton, T.J Everyone Loses (2017) The Ukraine Crisis and
the Ruinous Contest for Post-Soviet Eurasia Routledge/IISS
Freedman, L (2019) Ukraine and the Art of
Strategy Oxford University Press.
Wenu:
Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp).
Comments