TISHIO LA KIVITA KATI YA UKRAINE NA URUSI
RAIS wa Urusi Vladimir Putin ametangaza operesheni ya kijeshi katika eneo la Donbas nchini Ukraine
Akitoa tamko hilo katika hotuba ya televisheni leo asubuhi amewataka wanajeshi wa Ukraine waliopo katika eneo la mapigano mashariki mwa Ukraine kuweka silaha chini na kurejea majumbani mwao.
Aidha Saa chache baadaye milipuko ilisikika katika miji ya Odessa, Kharkiv, Kramatorsk, Mariupol and Kyiv Nchini Ukraine.
Naye Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema operesheni ya Russia imelenga kambi za jeshi za Taifa hilo hata hivyo Bunge la Ukraine limepitisha azimio la nchi hiyo kuwa katika hali ya hatari kwa siku 30 kutokana na mzozo uliopo kati ya Nchi hiyo na Urusi.
Mamlaka nchini humo zimeruhusiwa kuzuia raia kutoka, kuzurura na kuzuia Mikutano ya Vyama vya Siasa na Taasisi kwa maslahi ya Taifa.
Pia, Serikali imewalazimisha kujiunga na jeshi wanaume wote waliofikia umri wa kwenda vitani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amemtaka Rais wa Urusi, Vladimir Putin kurudisha Wanajeshi aliowapeleka Ukraine, akisema watu wengi wameshapoteza maisha na ni wakati wa kuipa nafasi Amani.
Aidha, Rais wa Marekani, Joe Biden amesema Urusi itabeba lawama kwa madhara yatakayotokea katika mzozo unaoendelea, akisisitiza Marekani pamoja na Washirika wake watajua cha kufanya.
Wakati taarifa za kuongezeka kwa idadi ya watu waliofariki baada ya Russia kuivamia Ukraine leo, viongozi mbalimbali duniani wametoa matamko ya kulaani uvamizi huo wakitaka usitishwe mara moja.
Karibu raia 10 na Wanajeshi 40 wa Ukraine wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Russia leo Alhamisi Februari 24, 2022 asubuhi katika mji wa Odessa ulio pwani ya Black Sea, Serikali imesema.
Taarifa zinasema zaidi ya Wanajeshi 40 na raia 10 wamefariki katika saa za mwanzo za uvamizi huo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliwaambia waandishi.
"Najua kwamba zaidi ya Wanajeshi 40 na maelfu wengine kujeruhiwa. Ninajua kuwa raia kumi wamepoteza maisha," amesema msaidizi wa Rais, Oleksiy Arestovych alipozungumza na waandishi.
Comments