IDADI YA VIFO YAFIKIA 26 KATIKA MLIPUKO LORI LA MAFUTA UGANDA
IDADI YA VIFO YAFIKIA 26 KATIKA MLIPUKO LORI LA MAFUTA UGANDA
Polisi wamesema idadi ya watu waliofariki katika ajali ya moto uliotokea baada ya mlipuko wa lori la mafuta eneo la Kigogwa kando ya Kampala-Bombo imefikia 26.
Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke amewaambia waandishi wa habari jana kuwa hadi kufikia tamati ya biashara siku ya Jumapili, idadi ya waliofariki ilikuwa bado 24, waathiriwa wengine wawili wamefariki.
"Kufikia jana jioni, waathiriwa wengine wawili walifariki katika hospitali ya Kiruddu na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 26," Kituuma alisema.
Alisema kati ya hao 26, 20 ni wanaume na sita ni wanawake.
Siku ya Jumapili, serikali ilianza mchakato wa kukabidhi miili ya marehemu kwa familia zao za karibu baada ya kufanya vipimo vya DNA ili kuwatambua waathiriwa.
Rusoke alisema kwa kuwa maiti hizo ziliteketea kiasi cha kutotambulika, polisi wanahitaji uchunguzi wa vinasaba (DNA) ili kusaidia kuwatambua pamoja na ndugu.
Alisema hadi sasa maiti 22 zimechukuliwa na ndugu wa marehemu huku zikiwa zimebaki nne tu.
Hivi majuzi serikali ilitangaza kuwa familia zilizoathiriwa zitapokea sh milioni moja kwa wale wanaopokea matibabu na sh milioni 5 kwa kila mmoja wa waliopoteza wapendwa wao.
Polisi bado wanachunguza hali ambayo lori la mafuta lililipuka baada ya kuhusika katika ajali na kuwaunguza watu kadhaa waliokuwa wamefika kuchomoa mafuta.
Wahanga wengine wengi walinaswa na moto huo ambao pia uliteketeza wafanyabiashara wa karibu, yakiwemo maduka katika mji wa Kigoogwa.
Imeripotiwa kuwa moto huo ulitokana na jiko la makaa lililokuwa karibu.

Comments