"HAKIKISHA VITA VINAISHA MWAKANI" ZELENSKY ANASUBIRI MPANGO WA TRUMP KUMALIZA VITA
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy tarehe 23 Novemba 2024 amesema kuwa anasubiri mapendekezo ya rais mteule wa Marekani Donald Trump kuhusu mpango wa kutatua mzozo unaoendelea kati yake na Urusi kwani alidokeza kuwa vita hivyo vinaweza kumalizika mwaka ujao.
Alisema vita hivyo vitaisha "wakati Urusi inataka viishe". "Wakati Amerika ina nafasi kubwa zaidi. Wakati Global Kusini iko upande wa Ukraine na upande wa kumaliza vita," alinukuliwa Zelenskyy akisema katika mkutano wa usalama wa chakula. "Haitakuwa njia rahisi, lakini nina imani kwamba tuna kila nafasi ya kuifanya mwaka ujao," Rais wa Ukraine aliongeza.
Alisema yuko wazi kwa mapendekezo kutoka kwa viongozi wa nchi za Kiafrika, Asia na Kiarabu. "Pia nataka kusikia mapendekezo ya rais mpya wa Marekani. Nafikiri tutayaona Januari na tutakuwa na mpango wa kumaliza vita hivi," alisema.
Zelenskyy alikuwa ameelezea matumaini wiki iliyopita katika mahojiano ya televisheni kwamba vita vitafikia mwisho "haraka" baada ya Trump kuanza muhula wake wa pili kama Rais wa Marekani. "Lazima tufanye kila kitu kuhakikisha kuwa vita vinamalizika mwaka ujao kwa njia za kidiplomasia," alisema.
Katika siku za hivi karibuni, Trump mara kwa mara ameibua maswali juu ya kuendelea kwa msaada wa Marekani kwa Ukraine. Wakati wa kampeni za uchaguzi, Trump mara nyingi alidai kwamba vita vya Urusi na Ukraine havingeanza kama angekuwa Rais. Alisema Julai mwaka huu atamaliza vita hiyo ndani ya siku moja baada ya kuchukua ofisi.

Comments