BENKI YA DUNIA KUTOA DOLA MILIONI 300 KUSAIDIA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASIKINI TANZANIA
Benki ya Dunia (WB) imeahidi kutoa Dola za Marekani Milioni 300 (takriban Tsh. Bilioni 779.9) kusaidia Awamu ya 3 ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF). Mpango huu unalenga kupunguza umaskini na kuongeza usawa wa kiuchumi nchini, ukilenga kaya zilizo katika mazingira magumu zaidi.
Kulingana na mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara ya Fedha jijini Dar es salaam Desemba 7, 2024 Awamu ya 3 ya mpango huo itakuwa ya kina zaidi na itaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoandaliwa kwa kipindi cha 2025-2050. Mpango huu unatarajiwa kuimarisha uwezo wa kaya masikini kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali, kuongeza kipato, na kupata huduma za kijamii.
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amebainisha kuwa hatua hii ni sehemu ya majadiliano yaliyofanyika kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia. Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Dkt. Nchemba alisema, “Uandaaji wa Mpango wa 3 wa TASAF utahusisha shughuli za uzalishaji, ambapo makundi yote ya kijamii yatahusishwa katika miradi ya maendeleo. Pia, kutakuwa na mgawanyo wa bajeti kwa shughuli maalum za maendeleo.”
Aidha, Waziri Nchemba amesisitiza kuwa mpango huo utazingatia ushirikishwaji wa makundi yote ya kijamii, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake, na watu wenye mahitaji maalum, ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote bila ubaguzi.
Benki ya Dunia imekuwa mshirika wa karibu wa Tanzania katika kutekeleza miradi ya kupunguza umaskini. Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya 3 unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa kijamii na kupunguza tofauti za kiuchumi kati ya kaya masikini na zile zenye kipato cha juu.

Comments