BUNGE LA AUSTRALIA LAPIGA MARUFUKU MITANDAO YA KIJAMII KWA WATOTO CHINI YA MIAKA 16
Bunge la Australia limepitisha sheria ya kwanza duniani inayozuia watoto chini ya miaka 16 kutumia mitandao ya kijamii kama TikTok, Facebook, na Instagram.
Aidha, Majukwaa yatakabiliwa na faini ya hadi dola milioni 50 za Australia ($33 milioni) kwa kushindwa kutekeleza marufuku hiyo.
Sheria hiyo imepitishwa na Seneti kwa kura 34 dhidi ya 19 na Baraza la Wawakilishi kwa kura 102 dhidi ya 13. Majukwaa hayo yatapewa mwaka mmoja kujiandaa kabla ya adhabu kuanza kutekelezwa.
Lengo kuu la kupitisha sheria hiyo ni kulinda watoto dhidi ya madhara ya mtandaoni, lakini wakosoaji wanahofia madhara yanayoweza kutokea, ikiwemo kutengwa kwa watoto walio katika mazingira magumu, athari kwa afya ya akili, na hatari kwa faragha ya watumiaji.
Aidha Majukwaa hayataruhusiwa kushurutisha watumiaji kutoa hati za utambulisho zilizotolewa na serikali ikiwa ni pamoja na pasipoti au leseni za udereva, wala kudai kitambulisho cha kidijitali kupitia mfumo wa serikali.
Wayne Holdsworth, ambaye mtoto wake wa kiume Mac alijiua baada ya kuangukiwa na kashfa ya ulaghai mtandaoni, alikuwa ametetea vizuizi vya umri na alijivunia kupitishwa kwa sheria hiyo. "Siku zote nimekuwa Mwaustralia mwenye fahari, lakini kwangu baada ya uamuzi wa leo wa Seneti, ninajivunia," alisema katika barua pepe.
Serikali inalenga kuongeza usalama wa watoto mtandaoni huku baadhi ya wataalam wakitaka sera zenye msingi wa ushahidi badala ya maamuzi ya haraka.

Comments