DK. SAMIA ASIKITISHWA NA AJALI YA MIKESE, MOROGORO
📌Asisitiza maelekezo aliyotoa Disemba 4, 2024 kufuatwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameonesha masikitiko makubwa kufuatia ajali mbaya iliyotokea usiku wa kuamkia leo, Desemba 18, 2024, ambapo watu 15 wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Ajali hiyo ilihusisha lori la mizigo na gari la abiria aina Coaster katika eneo la Mikese, Barabara Kuu ya Morogoro - Dar es Salaam.
Dk. Samia ametoa pole kwa familia za marehemu, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adam Malima, pamoja na ndugu, jamaa, na marafiki wa waathirika. “Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu ndugu zetu hawa wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka,” amesema Rais.
Akirejelea maelekezo aliyoyatoa Desemba 4, 2024, kuhusu kuongeza usimamizi wa Sheria za Usalama Barabarani, Dk. Samia amesema leo ameagiza Jeshi la Polisi kutekeleza hatua mpya kwa ajili ya kuimarisha usalama barabarani.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuanzishwa kwa mfumo wa Leseni za Udereva za Elektroniki, ambao utafuatilia makosa ya madereva na kupunguza alama (points) kwa madereva wanaofanya makosa ya hatari barabarani. Mfumo huu utaweka kumbukumbu za mwenendo wa madereva kielektroniki na kitakwimu, na kuamua iwapo wanastahili kuendelea kuwa na leseni za udereva au la.
Dk. Samia amesema mfumo huo ni sehemu ya maboresho ya mfumo wa sasa, ambao mara nyingi hukubali madereva kulipa faini pekee bila hatua za ziada, huku akisisitiza kuwa, “Uhai wa binadamu hauna mbadala, na hatuna budi kuendelea kuchukua hatua za pamoja na madhubuti kuhakikisha unalindwa kwa nguvu zote.”
Aidha, ameongeza kuwa ni lazima vyombo vya moto vinavyoingia barabarani vikaguliwe ili kuhakikisha vina sifa zinazotakiwa, na madereva wake wawe na rekodi nzuri na sifa zinazostahili kuendelea kuendesha.
Hili ni tamko la Rais lililojikita katika kuhakikisha usalama wa wananchi na kupunguza matukio ya ajali barabarani.

Comments