MADEREVA WAZEMBE 16,324 WAKAMATWA WAKATI WA SIKUKUU YA KRISMASI
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limefanikiwa kuwakamata madereva 16,324 waliobainika kukiuka sheria za usalama barabarani katika operesheni maalum zilizofanyika wakati wa sikukuu ya Krismasi.
Makosa yaliyojitokeza zaidi ni mwendo kasi, ulevi wakati wa kuendesha, kutovaa mikanda ya usalama, pamoja na magari mabovu yasiyokidhi viwango vya usalama. Operesheni hizi zililenga kupunguza ajali na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara katika kipindi hiki cha sikukuu.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, ACP Ramadhani Ng’anzi, amesema operesheni zitandelea katika msimu mzima wa sikukuu ili kuhakikisha madereva wanazingatia sheria na kanuni za usalama barabarani. Ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya madereva wanaopuuza sheria, kwani uzembe wao unaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.
Aidha, Kamanda Ng’anzi ametoa wito kwa madereva na abiria kufuata sheria na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kulinda maisha yao na ya watumiaji wengine wa barabara. Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi kuripoti ukiukwaji wowote wa sheria za usalama barabarani kwa lengo la kupunguza ajali na kuhakikisha usalama kwa wote.
Operesheni hizi zimeonyesha mafanikio makubwa katika kudhibiti uzembe barabarani na kupunguza hatari ya ajali katika msimu wa sikukuu.

Comments