NAIBU WAZIRI PINDA AIPONGEZA ARITA KWA UBUNIFU WA TAARIFA ZA KIJIOGRAFIA
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geophrey Mizengo Pinda (Mb.), amepongeza ubunifu wa utafiti wa taarifa za kijiografia uliobuniwa na wahitimu wa Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA).
Akizungumza katika mahafali ya 42 ya Chuo hicho yaliyofanyika Desemba 13, 2024, katika mtaa wa Ikulu, Kata ya Cheyo, Mkoani Tabora, Mhe. Pinda amesema kuwa ubunifu huo unaweza kuchochea maendeleo ya sekta ya ardhi nchini ikiwa utaratibu sahihi wa kuwawezesha wahitimu hao utaandaliwa.
Aidha, Mhe. Pinda ametoa wito kwa halmashauri zote nchini kuvitumia vyuo vya Ardhi Tabora na Morogoro katika kupanga matumizi ya ardhi, kupima viwanja, na kuvimilikisha kisheria. Alisisitiza kuwa, “Ardhi isiyopimwa na isiyomilikishwa kisheria ni sawa na mtaji mfu.”
Katika hotuba yake, Mhe. Naibu Waziri amewaasa wahitimu kuacha kabisa vitendo vya wizi, dhuluma, ubadhilifu, na kuomba au kupokea rushwa. Aliwataka kutumia ujuzi walioupata chuoni kwa manufaa ya umma, akisisitiza kuwa ardhi ni msingi wa maendeleo ya kila Mtanzania.
Katika chuo hicho jumla ya wahitimu 1,097 wametunukiwa Astashahada na Stashahada katika fani mbalimbali zikiwemo:
• Urasimu Ramani
• Usimamizi wa Ardhi
• Sanaa, Ubunifu na Uchapaji
• Usimamizi wa Mazingira
• Mifumo ya Tehama
Mahafali haya yanaonesha mchango mkubwa wa Chuo cha Ardhi Tabora katika kuzalisha wataalam muhimu kwa maendeleo ya sekta ya ardhi nchini.


Comments