RAIS SAMIA ATOA ZAWADI ZA KRISMASI KWA WATOTO YATIMA NCHINI KOTE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha upendo wake kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwa kutoa zawadi za Krismasi kwa vituo vya kulelea watoto nchini kote. Zawadi hizo zinalenga kuleta faraja na furaha kwa watoto hao katika msimu huu wa sikukuu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila Disemba 23, 2024 amekabidhi zawadi hizo akisema kuwa zimetolewa kuwafikia watoto yatima katika mikoa yote 26 ya Tanzania bara.
Zawadi hizo ni pamoja na mchele, maharage, mbuzi, na mahitaji mengine muhimu, ambazo zimekabidhiwa kwa vituo mbalimbali. Kwa mfano, katika Kituo cha Kulelea Watoto cha Msimbazi, Rais Samia alihakikisha watoto wanapata mahitaji yote ya kusherehekea Krismasi kwa furaha. Aidha, mkoa wa Iringa pia umefaidika na zawadi hizo, ambapo watoto walipokea vyakula na zawadi nyingine za sikukuu.
Vile vile alisisitiza kuwa hatua hii ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma, hususan wale wanaoishi katika mazingira magumu. “Watoto hawa ni sehemu ya familia yetu kubwa ya taifa, na ni wajibu wetu kuhakikisha wanasherehekea Krismasi kwa furaha na matumaini,” alisema
Hatua hii imepongezwa na wananchi wengi, ikionekana kama ishara ya mshikamano wa kitaifa na upendo kwa watoto wasiojiweza.
Serikali inaendelea kuhimiza Watanzania kushirikiana na kutoa msaada kwa wahitaji, hasa wakati wa msimu wa sikukuu.

Comments