SERIKALI YAKABIDHI NYUMBA 109 KWA WAATHIRIKA WA MAPOROMOKO HANANG


SERIKALI YAKABIDHI NYUMBA 109 KWA WAATHIRIKA WA MAPOROMOKO HANANG


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Disemba 20, 2024, imekabidhi rasmi nyumba 109 kwa waathirika wa maporomoko ya tope yaliyotokea Disemba mwaka jana wilayani Hanang, mkoani Manyara.



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi nyumba hizo kwa waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope yaliyotokea Desemba, mwaka jana wilayani Hanang, mkoani Manyara.

 

Akizungumza mara baada ya kukabidhi na kuzindua nyumba hizo zilizojengwa katika kitongoji cha Waret, Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara, Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapa pole waathirika wote na amesisitiza kuwa Serikali itawasaidia ili waendelee na maisha yao kama ilivyokuwa awali.

 

Amesema kuwa ujenzi wa nyumba 73 kati ya 109 umegharamiwa na Serikali Kuu na kujengwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT); nyumba nyingine 35 zimejengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, ilhali nyumba moja imejengwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UWT).

 

“Kufuatia maafa hayo, nyumba 109 zilihitaji kujengwa upya kwa haraka. Hivyo, kwa kuzingatia athari hizo, na kwa upendo wake, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alitoa maelekezo ya kujenga nyumba bora na za kudumu katika eneo salama kwa waathirika waliopoteza makazi yao. Ujenzi huu ni ishara ya kujali, upendo na dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa pamoja na wananchi wakati wa shida,” amesema.

 

Ameongeza kuwa, Rais Dkt. Samia alitoa kiasi cha shilingi bilioni 1.38 kwa ajili ya kuweka huduma za kijamii ikiwemo umeme, maji na barabara za uhakika; lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila nyumba inafikiwa na huduma hizo.

 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang waratibu zoezi la ugawaji wa viwanja vya ziada vilivyopo katika eneo hilo ili kuendeleza eneo hilo. “Tunataka eneo hili lisitambuliwe kama makazi ya waathirika, bali kijiji rasmi chenye huduma zote muhimu za kijamii na liwe kielelezo cha maboresho ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote.”

 

Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa miongozo, maono na fikra thabiti ya namna ya kukabiliana na kurejesha hali wakati yalipotokea mapororoko ya tope wilayani Hanang. “Ujenzi wa nyumba hizi ni maono yake, pia ameleta majiko ya gesi 109 ambayo watakabidhiwa wakazi wa eneo hili.”


Nyumba hizo zimejengwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi waliopoteza makazi yao kurejea katika hali ya kawaida ya maisha baada ya kukumbwa na janga hilo. Tukio hilo la kusikitisha lilipelekea baadhi ya wananchi kupoteza wapendwa wao pamoja na mali zao.


Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kusaidia wananchi katika nyakati za changamoto, huku ikiwasihi wanufaika wa nyumba hizo kuzijali na kuzitumia kwa uangalifu.


 

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA