TANZANIA IMEFANIKIWA KUFUNGUA SOKO LA ASALI CHINA
Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kufungua soko la asali nchini China, hatua muhimu inayolenga kukuza uchumi wa Tanzania na kuongeza mapato ya wafugaji nyuki.
Mnamo Agosti 15, 2024, Tanzania na China zilisaini Itifaki ya kuuza asali ya Tanzania nchini China. Soko la China lina idadi kubwa ya watu zaidi ya bilioni 1.4 na linaagiza zaidi ya tani milioni 38 za asali kila mwaka.
Katika utekelezaji wa makubaliano hayo, Serikali ilikusanya tani 10 za asali kwa ajili ya usafirishaji kwenda China. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastan Kitandula, alishuhudia kuagwa kwa kundi la kwanza la asali kabla ya kusafirishwa.
Aidha, Oktoba 4, 2024, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Pindi Chana, alizindua nembo ya asali ya Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora na ufanisi katika uzalishaji wa asali.
Nembo hii itasaidia kutambulisha na kukuza soko la asali ya Tanzania kimataifa.
Serikali pia imejenga viwanda sita vya kuchakata mazao ya nyuki katika Wilaya za Kibondo, Sikonge, Mlele, Nzega, na Bukombe ili kuhakikisha asali inayouzwa nje ya nchi inakuwa na viwango vya ubora vinavyokidhi mahitaji ya masoko hayo.
Kwa ujumla, hatua hizi zinatarajiwa kufungua fursa mpya za kibiashara kwa wafugaji nyuki na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa, huku ikilenga kuimarisha biashara ya kimataifa na kuongeza ajira.

Comments