BIASHARA SAA 24 YALETA MATUNDA SOKO LA MACHINGA
Biashara ya saa 24 imeonyesha mafanikio makubwa katika Soko la Machinga, ambapo bidhaa mbalimbali zimenunuliwa usiku na kuleta tija kwa wafanyabiashara katika soko hili maarufu. Ufanisi huu umeonyesha jinsi biashara hii inavyoweza kuboresha mazingira ya uchumi na kuongeza tija kwa wafanyabiashara.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, hivi karibuni alithibitisha kuwa mpango wa kufanya biashara kwa saa 24 katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, unatarajiwa kuanza rasmi hivi karibuni. Alisema tathimini inayofanywa na timu iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, inalenga kupunguza msongamano wa wafanyabiashara mchana na kutoa nafasi kwa wengine kufanya biashara usiku.
Mpogolo alieleza kuwa serikali inatarajia kuanza utekelezaji wa mpango huo mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Februari 2025. Alifafanua kuwa maandalizi yanaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wamiliki wa majengo, wadau wa usafiri, na Jeshi la Polisi, ili kuhakikisha usalama wa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Hatua muhimu zitajumuisha ufungaji wa taa na kamera za usalama katika maeneo ya biashara, na kuhamasisha wamachinga kuhamia kwenye maeneo yasiyoathiri shughuli za kijamii. Barabara kama Uhuru na maeneo yenye benki zitaendelea kuwa wazi kwa matumizi ya umma ili kuhakikisha huduma za kijamii zinaendelea bila usumbufu.
Mpogolo pia alieleza kuwa mitaa maarufu ya Kariakoo, kama Congo, Nyamwezi, na Sikukuu, itaendelea na shughuli zake kama kawaida. Alisema kuwa biashara ya saa 24 itatoa fursa kwa vijana wa usafirishaji kwa bodaboda na bajaji, hivyo kuhakikisha bidhaa zinawafikia wananchi kwa usalama na haraka, na pia kusaidia kukuza ajira na huduma bora kwa jamii.

Comments