HUDUMA ZA DHARURA NJE YA HOSPITALI KWA KUSHIRIKIANA NA WADAU KUIMARISHWA
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza mkakati wa kuimarisha huduma za dharura nje ya hospitali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, alipotembelea kampuni ya Emergency Medical Services inayofahamika kama E-Plus Tanzania, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam. Kampuni hiyo ni miongoni mwa watoa huduma za ambulance nchini.
Dkt. Jingu alisema kuwa E-Plus imekuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kuhakikisha huduma za dharura zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaohitajika.
“Nimewasikiliza na kupokea maoni yao kuhusu maeneo ambayo wanahitaji msaada kutoka Serikalini ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Kwa mujibu wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Serikali ina jukumu la kuwezesha sekta binafsi ili iweze kuchangia kikamilifu maendeleo ya huduma za afya, hususan huduma za dharura,” alisema Dkt. Jingu.
HUDUMA BORA ZA DHARURA
Katika ziara hiyo, Dkt. Jingu alitembelea na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na E-Plus Tanzania, ikiwemo:
• Chumba cha kupokea taarifa za dharura (Dispatch room): Hufanya kazi kwa saa 24 kwa siku, likiratibu maombi ya huduma za dharura na zisizo za dharura.
• Chumba cha vifaa vya huduma za dharura: Kituo hicho kimewekewa vifaa vya kisasa kwa ajili ya huduma za haraka.
• Ambulance za kisasa: Ambulance hizo zina vifaa vya kiwango cha juu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya huduma za wagonjwa mahututi (ICU inayotembea).
Dkt. Jingu alisifu jitihada za E-Plus Tanzania na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha huduma za dharura zinaimarika zaidi.
MSIMAMO WA E-PLUS TANZANIA
Mkurugenzi wa E-Plus Tanzania, Dkt. George Pondo, alisema kuwa kampuni hiyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kufanikisha malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya za dharura.
“Tunayo magari ya dharura ya kisasa yaliyo na vifaa bora vya huduma. Tuna nia ya dhati ya kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa sekta binafsi kutoa huduma bora kwa Watanzania wote. Haki ya kupata huduma ya ambulance ni ya kila Mtanzania, popote alipo,” alisema Dkt. Pondo.
KUIMARISHA MFUMO WA HUDUMA ZA DHARURA
Ziara hii ni sehemu ya mpango wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kukagua na kuimarisha utekelezaji wa mkakati wa kuboresha huduma za dharura nchini. Mkakati huo unalenga:
• Kuimarisha huduma za dharura nje ya hospitali kupitia magari ya wagonjwa.
• Kukuza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuratibu huduma za dharura.
Serikali imeweka msukumo maalum katika kuhakikisha huduma za dharura nchini zinapatikana kwa wakati, zenye ubora wa hali ya juu, na kuwafikia wananchi wote.


Comments