JAFO AANIKA MPANGO WA UJENZI WA VIWANDA 9,048


Waziri wa Viwanda na biashara Mhe. Dkt. Seleman Jafo ameweka wazi mpango wa serikali wa kujenga viwanda 9,048 kote nchini. 


Waziri Jafo alitoa kauli hiyo tarehe 2 Januari 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wa maendeleo ya viwanda uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Katika hotuba yake, Waziri Jafo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya mpango huo wa viwanda 9,048.


Mpango huu ni sehemu ya jitihada za kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.


Waziri Jafo alieleza kuwa viwanda hivyo vitahusisha sekta mbalimbali, ikiwemo usindikaji wa mazao ya kilimo, ufugaji, uvuvi, na uzalishaji wa bidhaa za viwandani. Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha kila halmashauri inajenga angalau viwanda vitano vinavyoendana na rasilimali zilizopo katika maeneo husika , amesema katika mwaka 2025 kipaumbele kikubwa ni pamoja na kuzindua mpango wa Miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030  wa ujenzi wa viwanda 9,048.

Mpango huu ndani ya miaka mitano utakwenda katika mikoa na mamlaka ya serikali za mitaa, lengo kuajiri watu milioni 6.5 ambao ni wastani wa watu zaidi ya milioni moja kwa mkupitia mpango huo utakwenda kutatua changamoto ya ajira, upatikanaji wa  malighafi na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinaongeza thamani nchini.


Aidha Dktl. Jafo amesema  biashara ni uti wa mgongo wa taifa  hivyo mwaka 2024 ulikuwa wa mafanikio zaidi  kwani Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara iliweza kuzindua sera ya biashara ya mwaka 2023, kuwa na mikakati ya pamoja ya jinsi ya ushiriki wa uchumi wa taifa pamoja na kuhamasisha wawekezaji kujiingiza zaidi katika suala la viwanda ili kutoa ajira kwani  Serikali pekee haiwezi kuajiri vijana wote wanaomaliza vyuo na si Serikali ya Tanzania tu hata nyinginezo duniani , hivyo ni lazima kuwa na sehemu nyingine mbadala ya kupata ajira hasa sekta binafsi kupitia viwanda.


Dkt.Jafo pia amesema Serikali ya Tanzania kwa mara ya kwanza ilisaini mkataba wa uwekezaji  Maganga Matitu wa uzalishaji wa chuma ambapo ni jambo kubwa sana kwani litafanya kupiga hatua kwa  sababu Tanzania inafanya uzalishaji wa chuma lakini viwanda vya chuma vina changamoto mbalimbali za kimiundombinu.


Vilevile Dkt.Jafo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ulipaji fidia ya sh. bilioni 15 katilka mradi wa Liganga na Mchuchuma baada ya kufanya tathmini, pia amesema Serikali itatengeneza kiwanda cha msingi cha utengenezaji wa magadi soda ambayo ni malighafi ya viwanda vingi.


Dkt.Jafo pia amewataka Watanzania kujua umuhimu wa kutumia bidhaa za ndani kuwawezesha vijana kupata ajira na kustawisha viwanda nchini na kuchangamkia soko huru la Afrika kwa zaidi ya nchi 50.






Kwa mujibu wa mpango huo:

Viwanda vya kilimo vitazingatia mazao kama mahindi, mpunga, na korosho.

Sekta ya ufugaji itajumuisha uzalishaji wa maziwa, nyama, na ngozi.

Sekta ya uvuvi itaweka mkazo kwenye usindikaji wa samaki na mazao ya baharini.


Waziri Jafo alisisitiza ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na wananchi katika kufanikisha mpango huu. Pia alibainisha kuwa serikali itatoa mafunzo kwa vijana na wanawake ili kuhakikisha wanapata ujuzi wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji viwandani.


Mpango huu unalenga kuongeza thamani ya mazao ya ndani, kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje, na kuinua uchumi wa taifa kupitia viwanda vidogo na vya kati. Serikali ina matumaini kuwa mpango huu utafungua ukurasa mpya wa maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA