KAMATI YA KANUNI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR NA ZHSF WAPONGEZA UBORESHAJI HUDUMA MUHIMBILI



Wajumbe Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogondogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) leo wametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufurahishwa na maboresho ya mifumo ya utoaji huduma ikiwemo miundombinu, mazingira ya utoaji huduma zenyewe pamoja na uwekezaji wa vifaa tiba.


Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mihayo Juma Nungu amesema baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hospitali wameona maboresho mengi na kujifunza namna ambavyo wataenda kuyatekeleza ili kuboresha zaidi utoaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi huko Zanzibar.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ZHSF Mhe. Mbarouk Omar Mohammed amesema wameona namna ambavyo wanachama wa Mfuko wa Taifa Bima ya Afya NHIF yenye uzoefu wa karibu miaka 25 na ZHSF yenye uzoefu wa zaidi ya mwaka mmoja wanavyohudumiwa hospitali hapo na kuongeza kuwa utoaji huduma unaenda vizuri na pale penye changamoto zinatatuliwa kwa wakati.


Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Rachel Mhaville amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa kwani hospitali hiyo ina uzoefu mkubwa wa kibobezi katika utoaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hivyo ni fursa kubwa ya kuboresha na kuimarisha ushirikiano katika utoaji huduma kwa pande zote mbili kwa manufaa ya wananchi na Serikali kwa ujumla.


Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF ambaye pia ni Meneja NHIF Mkoa wa Ilala, Dkt. Aifena Mramba amesema Julai 2024, NHIF iliingia makubaliano na ZHSF ili kuwezesha wanachama wake kupata huduma Tanzania bara kwa kutumia mifumo na taratibu za NHIF kulingana na makubaliano yaliyofanywa na pande hizo mbili hivyo wametembelea MNH kama moja wapo ya kituo cha huduma kujionea wenyewe utekelezaji wa makubaliano hayo.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA