KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE UTAWALA KATIBA NA SHERIA YAPOKEA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA
Tarehe 14 Januari 2025, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeendesha kikao maalum katika Jengo la Utawala, Bungeni Dodoma, kwa ajili ya kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2024.
Wajumbe wa Kamati hiyo walipokea maelezo ya kina kutoka kwa viongozi wakuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, akiwemo:
• Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria.
• Mhe. Jumanne Sagini, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria.
• Bw. Hamza Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika uwasilishaji wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alieleza umuhimu wa Muswada huu ambao unalenga kuboresha na kuoanisha sheria mbalimbali ili kuhakikisha kwamba mfumo wa sheria unaendana na mahitaji ya sasa ya kijamii na maendeleo ya taifa.
MAMBO MUHIMU KATIKA MUSWADA:
1. Marekebisho ya Kiutendaji: Kufanya mabadiliko yanayolenga kuondoa changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa sheria.
2. Uimarishaji wa Sheria za Kimkakati: Kuoanisha sheria za Tanzania na mazingira ya kimataifa ili kuchochea uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.
3. Masuala ya Haki za Kisheria: Kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa sheria.
Kikao hiki ni hatua muhimu ya mchakato wa kutunga sheria, ambapo Kamati inashirikiana na Wizara husika kuhakikisha kuwa marekebisho yanayopendekezwa yanazingatia maslahi ya taifa na yanakidhi mahitaji ya wananchi.
Muswada huu unatarajiwa kuwasilishwa rasmi kwa wabunge wote kwa ajili ya mjadala wa kina na kupitishwa. Hatua hii inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha mfumo wa sheria unakuwa wa kisasa na unawajibika kwa mahitaji ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Comments