MADAKTARI BINGWA WATOA HUDUMA KWA WANANCHI ZAIDI YA 2,000 TEMEKE
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke, Dkt. Joseph Kimaro, amesema kuwa zaidi ya wananchi 2,000 wamepata matibabu ya kibingwa katika kambi maalumu ya siku tano iliyofanyika hospitalini hapo.
“Wakati wa kambi hii maalumu, tumewahudumia jumla ya wagonjwa 2,442. Kati yao, wanawake walikuwa 1,478, sawa na asilimia 61, huku wanaume wakiwa 964, sawa na asilimia 39. Pia, watoto chini ya miaka mitano waliohudumiwa walikuwa 282,” alisema Dkt. Kimaro.
Aidha, Dkt. Kimaro alieleza kuwa kambi hiyo imebaini kuwa asilimia 63 ya wagonjwa waliohudumiwa walikuwa na magonjwa yasiyoambukiza, jumla yao ikiwa 1,538.
“Madaktari Bingwa 55 walihusika katika kutoa huduma mbalimbali za kibingwa, ikiwemo upasuaji kwa wagonjwa 59. Upande wa maabara ulifanya vipimo 1,861, huku huduma za radiolojia zikijumuisha vipimo 702, ikiwemo Ultrasound, CT Scan na X-ray,” aliongeza.
Kwa upande wake, Dkt. Bryceson Kiwelu, mmoja wa Madaktari Bingwa, aliwahimiza wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza, hasa kwa wanawake walioonekana kuathirika zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke, Dkt. Deus Buma, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanikisha zoezi hilo muhimu, akisema limewawezesha wananchi kupata huduma za matibabu kwa gharama nafuu.

Comments