MILIONI 600 KUIPANDISHA HADHI ZAHANATI YA SUJI KUWA KITUO CHA AFYA
Na WAF - Same, Kilimanjaro
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga shilingi Milioni 600 kwa ajili ya kuipandisha hadhi Zahanati ya Suji iliyopo Kijiji cha Malindi, Wilaya ya Same, Kilimanjaro kuwa Kituo cha Afya. Hatua hii inalenga kuongeza huduma za afya, ikiwemo huduma za kulaza wagonjwa na chumba cha upasuaji wa dharura.
Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, alitoa taarifa hiyo tarehe 8 Januari 2025, alipokuwa akikagua na kuzindua miradi ya afya mkoani Kilimanjaro. Alisema kuwa hatua ya kuipandisha hadhi zahanati hiyo itahakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na maeneo yao.
“Ni muhimu tukaongeza huduma za afya Suji kwa kuwa na wodi maalum za kulaza wagonjwa, chumba cha upasuaji, na huduma za mionzi. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha dhamira kubwa kwa kuleta maendeleo haya kupitia usimamizi bora wa rasilimali,” alisema Waziri Mhagama.
Zahanati ya Suji inahudumia wananchi wanaokabiliwa na changamoto ya kusafiri zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma za afya, ikiwemo huduma za kujifungua na upasuaji. Kukamilika kwa uboreshaji huu kutapunguza changamoto hizo.
Waziri Mhagama aliwahimiza wananchi wa Kijiji cha Malindi:
1. Kutunza miundombinu ya afya na mazingira.
2. Kuepuka uharibifu wa mazingira unaochangia mabadiliko ya tabianchi na milipuko ya magonjwa.
3. Kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa kwa kufuata ushauri wa wataalamu.
4. Kufuata mtindo wa maisha bora kwa kufanya mazoezi na kupunguza matumizi ya chumvi, sukari, na mafuta ili kuzuia magonjwa yasiyoambukiza.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia imeendelea kuweka mkazo kwenye kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha huduma zinapatikana kwa urahisi na ubora katika maeneo ya vijijini na mijini.


Comments