NOTI MPYA KUANZA KUTUMIKA FEBRUARI 2025


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emanuel Tutuba, ametangaza kuwa noti mpya za Tanzania zenye saini ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, na yeye mwenyewe zitaanza kutumika rasmi kuanzia Februari mwaka huu.


Noti hizi, ambazo ni za toleo la mwaka 2010, zitaingizwa kwenye mzunguko wa fedha ili kuboresha mfumo wa matumizi ya fedha nchini.


Gavana Tutuba ameeleza kuwa noti hizo mpya zitakuwa na viwango vyote vya thamani vinavyotumika sasa, ikiwa ni pamoja na Shilingi 500, 1,000, 2,000, 5,000, na 10,000. Aliongeza kuwa hatua ya kuzindua noti mpya inalenga kuimarisha usalama wa fedha za Tanzania kwa kutumia teknolojia za kisasa za uchapaji wa noti.


Aidha, Gavana ametoa wito kwa wananchi kutambua kuwa noti zilizopo kwa sasa zitaendelea kutumika sambamba na noti mpya hadi zitakapochakaa kiasili. “Hakutakuwa na ulazima wa kubadilisha noti zilizopo kwa sasa, kwani zitaendelea kuwa halali hadi pale zitakapotolewa rasmi kwenye mzunguko,” alisema.


Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amepongeza juhudi za Benki Kuu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na fedha za kisasa zinazozingatia viwango vya kimataifa. Pia alitoa wito kwa taasisi za fedha na benki kuhakikisha elimu kuhusu noti mpya inatolewa kwa wananchi.


Noti mpya zimetengenezwa kwa kuzingatia viwango vya usalama vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na vipengele vya kiusalama visivyoweza kuigwa, kama vile maandishi ya siri, alama za maji, na vipande vya metali vinavyoonekana kwenye mwanga wa jua.


Kwa sasa, Benki Kuu imeanza kampeni ya uhamasishaji kwa umma kuhusu noti mpya, ikiwemo kupitia vyombo vya habari na semina za elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii.


Taarifa zaidi kuhusu noti hizi na taratibu za matumizi zitaendelea kutolewa na Benki Kuu ya Tanzania.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA