POLISI KUANZA OPARESHENI KALI DHIDI YA MAGARI YA WANAFUNZI TAREHE 5 JANUARI 2025


Jeshi la Polisi limetangaza mpango wa kuanza oparesheni kali ya ukaguzi wa magari yanayobeba wanafunzi kote. 


Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu, tarehe 30 Desemba 2024, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dodoma. 


Kamanda Musilimu alibainisha kuwa oparesheni hiyo itaanza rasmi tarehe 5 Januari 2025, na itaendelea kwa muda usiojulikana hadi malengo ya kuimarisha usalama wa wanafunzi yatakapofikiwa.


Hatua hii inalenga kuhakikisha magari hayo yanazingatia sheria za usalama barabarani na kulinda maisha ya watoto wanaotegemea usafiri huo.


Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, ukaguzi huo utajumuisha:

Hali ya kiufundi ya magari ili kuhakikisha yako salama kwa matumizi.

Vibali vya madereva, ikiwa ni pamoja na leseni maalum za kuendesha magari ya wanafunzi.

Uwepo wa vifaa vya usalama kama mikanda ya viti na vifaa vya kuzima moto.


Oparesheni hiyo inakuja baada ya matukio kadhaa ya ajali zinazohusisha magari ya wanafunzi kuripotiwa, huku sababu nyingi zikihusishwa na uzembe wa madereva na ubovu wa magari.


Polisi wamesisitiza kuwa wamiliki wa magari hayo wanapaswa kufuata taratibu zote zilizowekwa ili kuepusha athari za kisheria. Vilevile, wazazi na walezi wanahimizwa kuwa makini na kuhakikisha magari wanayochagua kwa watoto wao yanakidhi viwango vya usalama.


Oparesheni hii inatarajiwa kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usalama barabarani na kupunguza hatari zinazowakabili wanafunzi wanaotegemea usafiri wa umma.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA