RAIS DKT. SAMIA AFUNGUA SHULE YA SEKONDARI MISUFINI ZANZIBAR
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 8 Januari 2025, amefungua rasmi Shule ya Sekondari ya Misufini, iliyoko Bumbwini, Zanzibar. Hafla hiyo ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Skuli ya Sekondari Misufini, iliyoko Bumbwini, Zanzibar, imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5. Shule hii ina madarasa 12 ya kisasa, maabara tatu za masomo ya sayansi, na maktaba yenye vifaa vya kujifunzia kwa teknolojia ya kisasa.
Kwa sasa, shule hii imeandikisha wanafunzi 450, huku ikiwa na uwezo wa kuchukua hadi wanafunzi 600 katika siku zijazo. Mradi huu ni sehemu ya juhudi za serikali ya Zanzibar kuboresha elimu kwa kuwekeza katika miundombinu bora na kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa Kizanzibari.
Rais Samia alibainisha kuwa shule kama hii zitachangia kuinua kiwango cha elimu kwa vijana, ambao ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza dhamira ya serikali katika kuboresha sekta ya elimu kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Pia amepongeza juhudi za serikali ya Zanzibar na wananchi wa Bumbwini kwa kushirikiana kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.
Shule hiyo inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha elimu kwa vijana wa eneo hilo, huku ikiwa na miundombinu ya kisasa inayowiana na mahitaji ya kisasa ya kujifunza.
Maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar yamepangwa kufikia kilele tarehe 12 Januari 2025.



Comments