RAIS DKT. SAMIA AZINDUA HOTELI YA KITALII YA NYOTA 5 ZANZIBAR, AJIRA ZAIDI YA 400 ZATARAJIWA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan leo Januari 7, 2025 ameizindua rasmi Hoteli ya Kitalii ya Bawe Island, inayomilikiwa na Cocoon Collection, katika Kisiwa cha Bawe, Zanzibar. Hoteli hii ya nyota tano, yenye vyumba zaidi ya 100, inatarajiwa kuleta ajira zaidi ya 450 kwa Watanzania, ikiwemo nafasi za ajira wakati wa ujenzi na uendeshaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa wawekezaji kuendeleza miradi yao kwa wakati. Pia ameunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, ya kuwapa miezi mitatu wawekezaji ambao hawajaanza ujenzi wa miradi yao visiwani, huku akionya kuwa visiwa vitarejeshwa serikalini ili kutafuta wawekezaji wapya.
Uwekezaji wa hoteli hii umegharimu dola za Marekani milioni 42 (takriban shilingi bilioni 104). Rais Samia alibainisha kuwa hoteli hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia ajira, mapato ya kodi, na kuvutia watalii wengi zaidi. Aidha, mradi huu unajumuisha miradi ya nishati jadidifu kama umeme wa jua na mifumo ya kuchuja maji ya chumvi kwa matumizi ya hoteli.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, alisisitiza faida za uwekezaji huo kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na fursa za ajira na soko la bidhaa za ndani. Wavuvi wa Zanzibar wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja kwa kuuza samaki kwa hoteli hiyo. Rais Mwinyi aliwataka wananchi kujiendeleza kielimu ili waweze kutumia fursa zinazotokana na ongezeko la hoteli na watalii Zanzibar.
Uzinduzi wa hoteli hii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuboresha sekta ya utalii na kuvutia wawekezaji zaidi visiwani humo.


Comments