SERIKALI KUJA NA MIFUMO YA HUDUMA ZA DHARURA RAFIKI NA WEZESHI KWA WATUMIAJI


Na WAF, Dar es Salaam


Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya huduma za dharura kwa kuanzisha mifumo ya mawasiliano ya kidigitali katika hospitali ya Taifa Muhimbili na nyinginezo nchini, ili kutoa huduma rafiki na wezeshi kwa watumiaji na kufikia lengo la kuokoa maisha.


Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, Januari 9, 2025, Jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea Mradi wa Kuimarisha Huduma za Matibabu ya Dharura katika hospitali ya Muhimbili. Dkt. Jingu alisema kuwa huduma za dharura ni muhimu kwa ustawi wa jamii, hasa katika kuokoa maisha pale zinapotokea changamoto kama ajali au magonjwa ya ghafla.


“Huduma za Dharura haziishii kwenye Ambulance tu, tunataka mtu anayepata dharura apokee huduma haraka na kwa ufanisi. Mfumo wa mawasiliano unahitaji kuimarika ili kuboresha matibabu ya dharura,” alisema Dkt. Jingu.


Amesisitiza kuwa, Serikali inaendelea kuboresha mifumo hiyo, na ni muhimu kuhakikisha vifaa vya dharura, ikiwa ni pamoja na magari ya wagonjwa, vinatumika ipasavyo kama ilivyoelekezwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Dkt. Jingu pia ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa jinsi inavyoshughulikia huduma za dharura kutoka hospitali mbalimbali, na kwa kutoa huduma bora kupitia Idara ya Tiba na Magonjwa ya Dharura na Kitengo cha Dharura kwa kina mama wajawazito.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA