SERIKALI YAJIPANGA KIKAMILIFU KUKABILIANA NA MARBURG


 

Serikali inaendelea na juhudi za kudhibiti ugonjwa wa Marburg tangu ulipotangazwa kwa mara ya kwanza Januari 19, 2025, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera.


Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe, alieleza Januari 24, 2025, kuwa wizara imeweka kambi wilayani humo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wahisiwa wa ugonjwa huo, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na kutambua dalili za ugonjwa huo. Mpaka sasa, idadi ya waliofariki ni wawili, wagonjwa wahisiwa ni 15, huku watu 281 waliokuwa karibu na waathirika wakiendelea kufuatiliwa.


“Serikali imeimarisha udhibiti wa ugonjwa huu kwa kuleta madaktari bingwa, vifaa vya upimaji, madawa, pamoja na kuwashirikisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii, ambao wanapita nyumba kwa nyumba kubaini wahisiwa wa ugonjwa huo,” alisema Dkt. Kapologwe.


Kwa mujibu wa Dkt. Kapologwe, wahudumu wa afya ngazi ya jamii 191 walioko kwenye mafunzo kwa vitendo wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za awali za matibabu kwa wananchi kwa weledi mkubwa. Kaya zote 10,893 katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo zimetembelewa, huku kata mbili kati ya 17 zikiripotiwa kuathirika.


Ameongeza kuwa maeneo 13 yametengwa kwa ajili ya wananchi waliokuwa karibu na waathirika, ambapo kati yao, 64 ni watumishi wa afya. Serikali pia inasambaza elimu kwa wananchi ili waepuke imani potofu kuhusu ugonjwa huo.


Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amepongeza jitihada zinazofanywa na wataalam wa afya kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya. Ametilia mkazo umuhimu wa elimu kwa wananchi ili waweze kujikinga.


“Wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni jeshi la awali la sekta ya afya, hivyo wanapaswa kutambua kuwa Serikali inawategemea katika kutatua changamoto za afya kwa jamii,” alisema Dkt. Magembe.


Aidha, amewasihi wananchi kuripoti mapema dalili zozote zisizo za kawaida kwenye vituo vya afya, huku akiwataka wahudumu wa afya kuzingatia uvaaji sahihi wa mavazi ya kujikinga dhidi ya maambukizi.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA