WAFANYABIASHARA KARIAKOO KUANZA KUREJESHWA SOKONI FEBRUARI 2025
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko Kariakoo, Mhe. Hawa Ghasia, amesema kuwa kazi ya kuwarejesha wafanyabiashara katika Soko la Kariakoo itaanza mapema Februari 2025.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika ukumbi mdogo wa TAMISEMI, Bi. Ghasia alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa soko hilo pamoja na uhakiki wa waliokuwa wafanyabiashara wake. Uhakiki huo ulifanywa na Timu Maalum iliyoundwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na wawakilishi wa wafanyabiashara, Menejimenti ya Shirika la Masoko ya Kariakoo, na vyombo vya usalama.
“Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika, ninapenda kuwajulisha wananchi na wafanyabiashara kuwa Soko la Kariakoo litaanza rasmi kurejesha shughuli zake kuanzia Februari 2025,” alisema Bi. Ghasia.
Aliongeza kuwa Menejimenti ya shirika hilo inaendelea kuratibu kazi ya kutangaza majina ya waliokuwa wafanyabiashara wa soko hilo ambao wamekidhi vigezo na sifa za kurejeshwa baada ya uhakiki. Jumla ya wafanyabiashara 1,520 wanatarajiwa kurejeshwa sokoni. Majina na fomu za kujiunga zitachapishwa kupitia vyombo vya habari pamoja na tovuti za Shirika la Masoko ya Kariakoo na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
“Nitoe wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote kuwa Shirika la Masoko ya Kariakoo, kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, litaendelea kutoa taarifa juu ya utaratibu wa kuelekea ufunguzi wa soko hili,” alihitimisha Bi. Ghasia.


Comments