WAKUU WA NCHI NA SERIKALI AFRIKA WAIPA KONGOLE TANZANIA KWA UZALISHAJI BORA WA MAZAO YA CHAKULA
Rais Museveni asifu ubora wa mchele wa Tanzania, atoa wito wa ushindani wa ubora.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wa Afrika wamepongeza hatua madhubuti zilizowekwa na Tanzania katika uzalishaji wa mazao ya chakula yenye ubora wa hali ya juu, hususan mpunga na mahindi.
Akizungumza leo (Jumamosi, Januari 11, 2025) kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika katika kituo cha mikutano cha Speke Resort, Munyonyo, Kampala, Uganda, Mheshimiwa Majaliwa alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha masuala ya utafiti, ushirikiano na sekta binafsi pamoja na taasisi za umma zinazojishughulisha na kilimo ili kuhakikisha inabaki kuwa kiongozi wa uzalishaji wa chakula barani Afrika.
Aidha, Waziri Mkuu alibainisha kuwa Tanzania imepokea kwa faraja kauli za viongozi wa Afrika, akiwemo Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, aliyesifu mchele wa Tanzania kwa ubora wake wa hali ya juu. “Haya ni mafanikio makubwa kwa sekta ya kilimo nchini,” alisema Waziri Mkuu.
Rais Museveni, wakati wa hotuba yake, alisema: “Natamani watu washindane kwa ubora katika uzalishaji wa mazao. Kwa mfano, mchele wa Tanzania ni bora zaidi na gharama yake ni nafuu. Kuna wakati walitaka nizuie usiingie nchini kwangu, lakini nikasisitiza ushindani wa bidhaa bora badala ya kuzuia.”
Kauli hiyo, kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, inatoa fursa kwa mataifa mengine barani Afrika kununua mazao ya chakula kutoka Tanzania, hasa mpunga.
Mheshimiwa Majaliwa alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kilimo hakibaki cha kujikimu pekee bali kinakuwa cha kibiashara. “Kwa sasa tunalenga kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na kuuza ziada nje ya nchi.”
Kwa upande mwingine, Rais Museveni alitoa wito kwa viongozi wa Afrika kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza ili kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana. Alitoa mfano wa zao la kahawa nchini Uganda, ambalo kilo moja ya kahawa ghafi huuzwa kwa dola mbili za Marekani, lakini baada ya kuchakatwa huuzwa kwa dola 40.
Kwa ujumla, mkutano huo ulilenga kuimarisha ushirikiano wa kilimo barani Afrika kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo Barani Afrika (CAADP 2026-2035) ili kuhakikisha Afrika inakuwa na uhakika wa chakula na inashindana katika soko la kimataifa.


Comments