WAZIRI NDUMBARO NA BALOZI WA URUSI WAJADILI USHIRIKIANO WA KISHERIA NA KIMAENDELEO


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro,  Januari 13, 2025, amekutana na Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Andrey Evetisyan, katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalihusu kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika sekta za kisheria na kimaendeleo.


Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), ambayo imelenga kuwasaidia wananchi kupata haki zao kisheria katika mikoa mbalimbali nchini. Waziri Ndumbaro alieleza mafanikio ya kampeni hiyo na jinsi ilivyoleta mabadiliko chanya kwa wananchi, hasa wale waliokosa fursa ya kupata msaada wa kisheria hapo awali.


USHIRIKIANO WA KIMAENDELEO


Mhe. Ndumbaro alimshukuru Balozi Andrey kwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili, huku akipendekeza kuendeleza juhudi za pamoja katika kuboresha mifumo ya kisheria kupitia mafunzo, teknolojia, na nyenzo za kisasa. Aidha, viongozi hao walijadili fursa za Urusi kushirikiana na Tanzania katika miradi ya elimu ya sheria, ikiwa ni pamoja na kubadilishana wataalamu na wanafunzi wa sheria.


Balozi Andrey alisisitiza nia ya Urusi kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania, hususan kupitia kampeni na mipango ya kisheria inayolenga kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Mazungumzo hayo yamefungua milango mipya ya ushirikiano baina ya Tanzania na Urusi, huku yakitoa matumaini ya kuimarisha huduma za kisheria kwa wananchi na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.


 

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA