WAZIRI WA AFYA APONGEZA USHIRIKIANO WA TANZANIA NA CHINA, APOKEA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA TZS MILIONI 125
Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, amepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya TZS Milioni 125 kutoka Serikali ya Watu wa China. Msaada huu unalenga kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kukabiliana na changamoto za utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Katika hafla ya makabidhiano, Mhe. Mhagama amesema msaada huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China. Alibainisha kuwa ushirikiano huu unazidi kuimarika kupitia maboresho ya huduma za afya, upatikanaji wa wataalamu mabingwa na vifaa vya kisasa vya teknolojia ya hali ya juu.
“Naupongeza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kusimamia vyema ushirikiano huu. Msaada huu utachochea maendeleo katika sekta ya afya na kuleta matokeo bora kwa wananchi,” alisema Mhe. Mhagama.
Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, aliishukuru Wizara ya Afya na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana kwa karibu na madaktari wa China waliopo nchini. Alisisitiza kuwa China itaendelea kuwa mshirika thabiti wa Tanzania katika kuboresha sekta ya afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi, alitoa shukrani kwa Serikali ya China na kueleza kuwa msaada huo utasaidia madaktari wa Tanzania kupata mafunzo ya kisasa nchini China.
“Ushirikiano huu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya rasilimali watu na matumizi ya teknolojia za kisasa kwa ajili ya utoaji wa huduma bora za afya,” alisema Prof. Janabi.

Comments