WAZIRI WA ULINZI NA JKT AKUTANA NA MWAKILISHI WA JUMUIYA YA ULAYA KUJADILI MASUALA YA USALAMA
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), amefanya mazungumzo Januari 17, 2025, na Balozi Johan Borgstam, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Ulaya (EU) katika nchi za Maziwa Makuu, ofisini kwake jijini Dodoma.
Balozi Borgstam, aliyefuatana na ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, alieleza utayari wa EU kushirikiana na Tanzania pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kukabiliana na changamoto za usalama na amani kwenye maeneo ya Maziwa Makuu, ambako Tanzania inashiriki kikamilifu.
“Tanzania imekuwa mshirika mkubwa wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya maendeleo na usalama,” alisema Balozi Borgstam.
Kwa upande wake, Waziri Dkt. Tax alimshukuru Balozi Borgstam kwa kutambua mchango wa Tanzania katika kulinda amani duniani na akasisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na EU kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika maeneo yenye changamoto za usalama.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na viongozi waandamizi wa Wizara ya Ulinzi na JKT, wakiwemo Rear Admiral Michael Mumanga, Mkurugenzi wa Maendeleo na Utafiti wa Wizara hiyo, pamoja na Meja Jenerali Naziad Mkeremy, Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).


Comments