WIZARA YA AFYA YATOA MWONGOZO KWA WASAFIRI KUFUATIA MLIPUKO WA UGONJWA WA MARBURG
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Afya, imetangaza Mwongozo Na. 15 wa tarehe 21 Januari 2025 baada ya kuthibitisha mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Marburg (MVD) katika Wilaya ya Biharamulo, Mkoa wa Kagera. Wilaya hiyo ipo umbali wa kilomita 1,450 kutoka Dar es Salaam na kilomita 1,068 kutoka Arusha.
Katibu Mkuu Wizara ya afya Dkt. Seif A. Shekalagne
amesema Mwongozo huu unalenga kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kudhibiti mlipuko na kuzuia usambazaji wa ugonjwa huo ndani na nje ya nchi, kwa kuzingatia Kanuni za Afya za Kimataifa za mwaka 2005.
HATUA ZA KUDHIBITI NA KUZUIA USAFIRI:
1. Fomu za Ufuatiliaji
Wasafiri wote wanaotoka Mkoa wa Kagera wanatakiwa kujaza fomu ya ufuatiliaji wa wasafiri kupitia mtandao kwa anuani https://afyamsafiri.moh.go.tz.
2. Ufuatiliaji wa Waliokaribu na Wagonjwa
Watu wote waliokuwa karibu na mgonjwa wa Marburg watafuatiliwa kwa ukaribu na hawataruhusiwa kutoka maeneo ya kujitenga hadi wapate kibali rasmi kutoka mamlaka za afya.
3. Ukaguzi Mipakani
Katika viwanja vya ndege, bandari, na mipaka ya nchi kavu, wasafiri wote watapimwa joto la mwili. Wasafiri watakaobainika kuwa na homa watapokea uchunguzi zaidi na matibabu yanayohitajika.
4. Elimu na Ushauri wa Afya
Taarifa na elimu kuhusu dalili za ugonjwa wa Marburg zitatolewa mipakani. Wasafiri wanashauriwa kuripoti dalili zozote kupitia namba ya bure ya simu 199.
5. Hatua za Kujikinga
Wasafiri na wafanyakazi katika mipaka wanapaswa kuzingatia hatua za kujikinga na maambukizi ikiwa ni pamoja na:
• Kunawa mikono mara kwa mara.
• Kutumia vitakasa mikono vyenye pombe.
• Kuepuka kusogeleana kimwili.
• Kuripoti dalili zozote za ugonjwa kwa mamlaka husika.
6. Wajibu wa Wasimamizi wa Usafiri
Wasimamizi wa vyombo vya usafiri wanatakiwa kuhakikisha:
• Uchunguzi wa afya wa abiria unafanyika mipakani.
• Vyombo vya usafiri vinawekwa safi na vinasafishwa mara kwa mara.
• Wanatoa taarifa mara moja kuhusu abiria yeyote mwenye dalili za ugonjwa kwa mamlaka za afya.
Taarifa Muhimu: Mwongozo huu wa wasafiri utahuishwa mara kwa mara ili kuendana na hali ya mlipuko na mahitaji ya kiafya.

Comments