ZAIDI YA ASILIMIA 97 YA WATU WAPATIWA DAWA ZA KINGATIBA YA MATENDE NA MABUSHA NCHINI
Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kuwapatia dawa za kingatiba ya matende na mabusha kwa wananchi 257,358 kati ya walengwa 265,217, sawa na asilimia 97, katika Halmashauri za Mtama na Mtwara Mikindani kwa mwaka 2024. Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kudhibiti na kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini.
Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, ametoa takwimu hizo Januari 30, 2025, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Tuungane, Tuchukue Hatua, Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele.”
Kwa upande wa ugonjwa wa usubi, watu milioni 5,462,851 kati ya milioni 6,447,157 kutoka halmashauri 24 walipatiwa kingatiba, ikiwa ni sawa na asilimia 85 kwa mwaka 2024.
Aidha, kuhusu ugonjwa wa trakoma, Waziri Mhagama amebainisha kuwa watu milioni 1,603,425 kati ya milioni 1,967,143 kutoka hadi halmashauri saba (Ngorongoro, Monduli, Longido, Kiteto, Simanjiro, Mpwapwa na Kalambo) walipatiwa kingatiba, sawa na asilimia 82.
Katika juhudi za kutibu ugonjwa wa minyoo ya tumbo, watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 14 wapatao milioni 9,896,694 walilengwa kupatiwa kingatiba, ambapo hadi kufikia Desemba 2024, watoto 8,676,234 sawa na asilimia 88, walimeza dawa hizo.
Kwa ugonjwa wa kichocho, walengwa walikuwa watoto milioni 8,145,947, kati yao watoto milioni 6,289,884 sawa na asilimia 77, walimeza dawa hizo katika halmashauri 171, sawa na asilimia 93 ya halmashauri zote nchini.
Katika huduma za tiba, mwaka 2024 watu 1,084 walifanyiwa upasuaji wa mabusha, huku wagonjwa 2,412 sawa na asilimia 67 ya matarajio, waliokuwa na tatizo la vikope wakifanyiwa usawazishaji wa kope bila malipo.
Waziri Mhagama ameipongeza timu ya watumishi wa serikali na wadau wa sekta ya afya kwa kazi nzuri ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za kingatiba kwa magonjwa haya. “Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 38 kati ya mwaka 2021 hadi 2024 kupitia mapato ya ndani, ili kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kutolewa bila malipo kwa wananchi,” amesema.
Amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi pindi mazoezi ya utoaji kingatiba yanapotangazwa kwenye maeneo yao ili kusaidia kutokomeza kabisa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini.

Comments