MOI KUANZA USAJILI WA WAGONJWA KWA KUTUMIA NAMBA YA NIDA KUANZIA FEBRUARI 1
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imetangaza kuwa kuanzia tarehe 1 Februari 2025, usajili wa wagonjwa utaanza kufanyika kwa kutumia namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA).
Hatua hii inalenga kuboresha mfumo wa utambuzi wa wagonjwa, kuhakikisha upatikanaji wa taarifa zao kamili, na kuweka kumbukumbu sahihi kwa uboreshaji wa huduma za afya. Pia, itarahisisha usomaji na ubadilishanaji wa taarifa za mgonjwa kati ya taasisi mbalimbali za matibabu, kupunguza mkanganyiko wa taarifa, na kusaidia ndugu kumtambua mgonjwa endapo atashindwa kujitambulisha.
Menejimenti ya MOI imewataka wagonjwa wote wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu kuhakikisha wanakuwa na Kitambulisho cha Taifa. Kwa wale ambao bado hawajapata kitambulisho hicho, watalazimika kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka Serikali ya Mtaa, Sheha, au Kijiji wanachoishi. Uwasilishaji wa barua hizo utafanyika hadi tarehe 30 Juni 2025.
MOI inawahimiza wananchi kuchukua hatua mapema ili kuepusha usumbufu wakati wa kupata huduma za matibabu.

Comments