WAKANDARASI WAJENGE BARABARA ZA TACTIC KWA WAKATI – MHANDISI MATIVILA
NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amewataka wakandarasi wanaojenga barabara za Engosheraton, Olasiti, na Oljoro jijini Arusha kuhakikisha zinakamilika kwa wakati ili kuwezesha maendeleo ya miundombinu katika jiji hilo.
Mhandisi Mativila alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake kwenye barabara hizo, ambazo zinajengwa kupitia Mradi wa Kuboresha Miji (TACTIC) chini ya TARURA. Barabara hizo zina urefu wa kilomita 12.1 na thamani ya shilingi bilioni 15.4, lakini utekelezaji wake bado uko nje ya muda uliopangwa.
“Barabara hizi zinapaswa kuwa zimefikia asilimia 99 ya ujenzi, lakini hadi sasa kazi haijakamilika. Wakandarasi lazima wahakikishe mradi huu unakamilika ifikapo Juni mwaka huu,” alisema Mhandisi Mativila.
Aliongeza kuwa barabara ya Oljoro bado ipo nyuma kwa asilimia 35 kutokana na mabadiliko ya usanifu wake, kwani sasa imepandishwa hadhi kuwa barabara ya mkoa kutokana na uwepo wa stendi mpya ya mabasi inayojengwa katika eneo hilo.
“Barabara hii itakuwa kiunganishi muhimu cha barabara kuu inayokwenda Dodoma. Tunapaswa kuongeza kasi ya ujenzi, hasa kwa kuwa mvua zinatarajiwa kunyesha muda wowote,” aliongeza.
WAKANDARASI WASISITIZWE UBORA NA KASI
Mhandisi Mativila alisisitiza kuwa mradi huu wa barabara tatu unapaswa kukamilika haraka lakini kwa kuhakikisha ubora wake, kwani serikali imewekeza fedha nyingi kwa maendeleo ya miundombinu.
“Sijaridhika na hatua ya utekelezaji wa mradi huu. Changamoto zilizopo zinapaswa kurekebishwa haraka. Serikali haitakubali ucheleweshaji wa miradi muhimu kwa wananchi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mhandisi John Benedict, msimamizi wa mradi kutoka kampuni ya Mhandisi Consultant Ltd, aliahidi kuwa barabara hizo zitakamilika ifikapo Juni mwaka huu na kwamba wataongeza nguvu kazi ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati.
Aidha, Mhandisi Sofa Edward kutoka Jiji la Arusha, ambaye anasimamia utekelezaji wa mradi huo, alibainisha kuwa watahakikisha wakandarasi wanamaliza kazi kwa muda uliopangwa ili wananchi wa kata husika waweze kufaidika na barabara hizo kwa urahisi wa usafiri na maendeleo yao.

Comments