RAIS DKT. SAMIA KUANDIKA HISTORIA KWA KUPATA TUZO YA KIMATAIFA KWA MAFANIKIO MAKUBWA KATIKA SEKTA YA AFYA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kupokea tuzo ya kimataifa ya The Gates Goalkeepers Award, ikiwa ni ishara ya kutambua mafanikio makubwa aliyoyapata katika uongozi wake, hususan katika kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi.


Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa Demografia na Afya ya mwaka 2022, Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya uzazi kwa asilimia 80, mafanikio yanayoifanya kuwa moja ya nchi zinazopiga hatua kubwa katika kuboresha afya ya mama na mtoto.


Akizungumza jijini Dar es Salaam Februari 3, 2025, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, alisema kuwa tukio hilo la utoaji wa tuzo linaloratibiwa na Taasisi ya The Gates Foundation litafanyika kwa mara ya kwanza nje ya Marekani, na Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji. Rais Samia Suluhu Hassan anakuwa kiongozi wa kwanza barani Afrika kupokea tuzo hiyo, hatua inayodhihirisha kutambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya afya na ustawi wa jamii.


“Hii ni heshima kubwa kwa Tanzania. Mataifa makubwa duniani yametambua juhudi za Rais Samia katika kuimarisha sekta ya afya, hasa kupitia mikakati madhubuti inayowezesha upatikanaji wa huduma bora kwa akina mama na watoto,” alisema Waziri Mhagama.


Alieleza kuwa mafanikio haya yamechangiwa na uongozi imara wa Rais Samia, ambao umeweka mazingira wezeshi ya kisera, kuongeza rufaa za akina mama na watoto, pamoja na kuboresha miundombinu ya huduma za afya kwa kiwango kikubwa.


“Rais Samia ameongeza bajeti ya sekta ya afya ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, na huduma za dharura kwa kina mama wajawazito. Kupitia jitihada zake, zaidi ya vituo 530 vya upasuaji wa dharura kwa ajili ya kujifungua vimejengwa nchini, hatua ambayo imeokoa maisha ya maelfu ya akina mama na watoto wachanga,” alifafanua Waziri Mhagama.


Aidha, Waziri alitoa pongezi kwa Taasisi ya The Gates Foundation kwa kutambua jitihada za serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya vifo vya akina mama, watoto wachanga, na watoto walio chini ya miaka mitano.


“Tunampongeza kwa dhati Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti katika kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaboreshwa. Tanzania ina kila sababu ya kujivunia juhudi hizi ambazo zimeipeleka nchi yetu kwenye ramani ya dunia kwa mafanikio makubwa,” alisema Waziri Mhagama.


Tuzo ya The Gates Goalkeepers Award ni moja ya tuzo zenye hadhi ya juu zinazotolewa kila mwaka kwa viongozi na watu mashuhuri duniani waliotoa mchango mkubwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa. Upokeaji wa tuzo hii unazidi kuiweka Tanzania katika nafasi ya kimataifa kama nchi inayopiga hatua kubwa katika sekta ya afya na ustawi wa jamii.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA