RAIS SAMIA AZINDUA SERA MPYA YA ELIMU, AZITAKA WIZARA HUSIKA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WAKE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa uwepo wa Sera Mpya ya Elimu na Mitaala Mipya pekee haviwezi kuleta matokeo chanya bila utekelezaji makini.
Akizungumza Februari 1, 2025, jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 – Toleo la 2023, Rais Samia ameagiza wizara husika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sera hiyo unafanyika kikamilifu ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Naitaka Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na TAMISEMI kuwezesha na kusimamia utekelezaji wa sera na mitaala hii mpya kwa ufanisi,” amesema Rais Samia.
MAGEUZI KATIKA SEKTA YA ELIMU
Katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza kuwa maboresho hayo lazima yawazingatie walimu kwa kuwapatia mafunzo sahihi, kuwaajiri wenye sifa stahiki, na kuboresha maslahi yao.
Aidha, ameweka wazi kuwa dhamira ya mabadiliko haya ni kumuandaa kijana mwenye kujiamini na aliye tayari kushindana katika soko la ajira la kikanda na kimataifa, huku akitumia rasilimali zilizopo nchini kwa manufaa yake na taifa.
“Kwa muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuongeza Pato la Taifa hadi kufikia Dola bilioni 700, ni wazi kuwa Sera hii itakuwa nyenzo muhimu ya kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa kuchochea uchumi wa nchi,” amesema Rais Samia.
Sera hii mpya imejikita pia katika elimu ya ujuzi na ujasiriamali, ambapo somo la ujasiriamali litafundishwa kwa kina ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuanzisha na kuendesha biashara zao. Vilevile, ujuzi na stadi zinazopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo zitatambuliwa na kurasimishwa.
MSISITIZO KATIKA ELIMU YA LUGHA ZA KIMATAIFA
Ili kuwaandaa vijana kushindana kikanda na kimataifa, Sera hii mpya pia imeweka mkazo katika ujifunzaji wa lugha mbalimbali za kimataifa, mbali na Kiingereza. Miongoni mwa lugha zitakazofundishwa ni Kichina, Kifaransa, na Kiarabu, ambazo ndizo zinazoendesha biashara na uchumi duniani.
VIONGOZI WENGINE WAZUNGUMZA
Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Sera ya Elimu ni mwongozo muhimu wa kuhakikisha maendeleo ya sekta hiyo yanaendana na malengo ya kitaifa.
“Sera hii mpya itatuwezesha kubadili mfumo wetu wa elimu ili kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa kumudu mabadiliko ya teknolojia,” amesema Dkt. Mpango.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, ameeleza kuwa chimbuko la mageuzi haya makubwa ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alianzisha mchakato huu kwa lengo la kuboresha elimu ya Tanzania kwa viwango vya kimataifa.
“Mabadiliko mengi serikalini huanzia kwa wataalam na mawaziri kabla ya kufika kwa Rais, lakini katika hili, Rais mwenyewe ndiye aliyekuwa wa kwanza kusukuma ajenda hii kwa nguvu zote,” amesema Prof. Mkenda.
Kwa uzinduzi wa sera hii mpya, Tanzania inaingia katika zama mpya za elimu zinazozingatia ujuzi, ubunifu, na ushindani wa kimataifa. Mafanikio ya sera hii yatategemea usimamizi madhubuti wa utekelezaji wake, hasa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu na maendeleo.

Comments