SERIKALI YAELEZA GHARAMA ZA KUUNGANISHA UMEME VIJIJINI


Dodoma, 30 Januari 2025 – Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amesema kuwa gharama ya kuunganisha umeme katika maeneo ya vijiji ni Shilingi 27,000, huku maeneo ya vijiji mji gharama ikiwa Shilingi 360,960.


Mhe. Kapinga alitoa ufafanuzi huo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukene, Mhe. Selemani Zedi, aliyependa kufahamu kwa nini maeneo ya Bukene na Itobo hayaunganishiwi umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000.


“Mheshimiwa Spika, maeneo ya Bukene na Itobo ni vijiji mji, hivyo yanafuata gharama ya Shilingi 360,960,” alisisitiza Mhe. Kapinga.


Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuona uwezekano wa kufanya maboresho ya gharama hizo. Aidha, tayari amemuagiza Meneja wa Mkoa wa Tabora na wa Wilaya ya Nzega kufanya tathmini ya kina ili kuondoa mkanganyiko uliopo kuhusu gharama za uunganishaji wa umeme katika maeneo hayo.


Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakari Asenga, aliyependa kufahamu kwa nini wakazi wa Katinduka bado wanalipa Shilingi 360,960 licha ya kuwa eneo la kijiji, Mhe. Kapinga alifafanua kuwa maeneo yanayounganishwa kwa Shilingi 27,000 ni yale yaliyopo kwenye mpango wa Serikali kwa kushirikiana na wafadhili wa miradi ya umeme vijijini. Alibainisha kuwa sio kila eneo linakidhi vigezo hivyo, na kwamba Katinduka ni eneo la mtaa, si kijiji.


Vilevile, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Anatropia Theonest, kuhusu lini vijiji vilivyobaki katika Wilaya ya Kyerwa vitapata huduma ya umeme, ikiwemo vijiji vya Buganza na Nyarigongo, Mhe. Kapinga alisema kuwa umeme umeshafika katika makao makuu ya vijiji hivyo, na mkandarasi anaendelea na kazi ya kusambaza umeme katika kilometa mbili za ziada.

Comments

Popular posts from this blog

RAIS SAMIA AHIMIZA MALEZI BORA KWA WATOTO

SERIKALI YAHAKIKISHA USAFIRI BORA BRT AWAMU YA PILI

RAIS WA CABO VERDE ASISITIZA UTAWALA BORA NA ULIPAJI FIDIA KWA AFRIKA KATIKA UFUNGUZI WA MWAKA MPYA WA MAHAKAMA YA AFRIKA JIJINI ARUSHA