SERIKALI YAZIDI KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA AKILI KWA KULETA MAPINDUZI KATIKA MAFUNZO NA AJIRA ZA WATAALAM
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wataalam wa afya ya akili nchini kwa kuwajengea uwezo wataalam 2,980 kutoka vituo 710 vya afya kote nchini ili waweze kutoa huduma hizo kwa ufanisi katika maeneo yao.
Hatua hii inalenga si tu kuongeza idadi ya wataalam waliobobea katika afya ya akili, bali pia kuhakikisha kuwa huduma hizo zinapatikana kwa urahisi katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya, hususan kwa wananchi walioko vijijini.
Akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Jonathani Msambatavangu, Bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Serikali inaendelea kupanua sekta ya afya ya akili kwa kuajiri wataalam zaidi na kuimarisha mafunzo kwa madaktari na wahudumu wa afya.
“Kwa mwaka 2024 pekee, Serikali imeajiri jumla ya watumishi wapya 56 katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, ikiwa ni jitihada za kupunguza uhaba wa wataalam wa sekta hii muhimu,” alisema Dkt. Mollel.
Katika jitihada za kuongeza wataalam waliobobea, Serikali imeendelea kutoa fursa za mafunzo ya juu kwa madaktari wa afya ya akili. Kwa kipindi cha miaka mitano (2020-2024), madaktari 61 wamepata nafasi ya kusomea udaktari bingwa wa afya ya akili, pamoja na ubingwa bobezi katika fani hiyo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa matibabu na huduma kwa wagonjwa wa afya ya akili.
Pamoja na hayo, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa elimu ya afya ya akili kwa kuongeza idadi ya vyuo vinavyotoa shahada ya uzamili katika fani hiyo. Dkt. Mollel alibainisha kuwa vyuo hivyo vimeongezeka kutoka kimoja mwaka 2019 hadi viwili ifikapo mwaka 2025, hatua ambayo itaongeza idadi ya wataalam wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta hiyo.
Hatua hizi zinadhihirisha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya ya akili, huku ikionyesha uwekezaji mkubwa katika sekta hii muhimu kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Comments